Sayari (kwaKiingerezaplanet) nikiolwa kikubwa cha angani kinachozungukajua (au nyota nyingine) na kung'aa kutokana nanuru ya jua iliyoakisiwa, tofauti nanyota na jua zinazong'aa peke yake. Kwamacho inaonekana kama nyota, lakini baada ya kuitazama kwa muda wamwaka inaonekana inabadilisha mahali pake angani, tofauti na nyota kwa jumla. Tofauti kubwa kati ya sayari nanyota ni kwamba, nyota ukiitazama inametameta ila sayari haiwezi.
Jina
Jina laKiswahili "sayari" linaasili yake katikaneno laKiarabuكوكب سيارkaukab sayar "nyota inayosogea"[1]. Neno hilo la Kiarabu linalingana au nitafsiri ya neno laKigiriki πλανήτηςplanetes (lenye maana ya "yenye kusogea") ambalo ni asili ya jina "planet" kwaKiingereza nalugha nyingine zaUlaya.
Tangu zamani watazamaji waanga katikatamaduni mbalimbali walitambua ya kwamba nyota kwa kawaida hukaa mahali pamoja lakini nyota chache zinabadilisha polepole mahali pake kati ya nyota nyingine zikifuatanjia zinazorudia kilamwaka. Nyota hizo ziliitwa "nyota zinazosogea".
Ufafanuzi wa sayari
Zamani kulikuwa na sayari5 tu zilizoonekana angani kwa macho matupu kama nyota zinazobadilisha mahali[2]. Tangu kupatikana kwa mitambo kamadarubini miaka 400 iliyopita idadi ya violwa angani vyenye miendo ya pekee imeongezeka sana lakini imeonekana pia kuna tofauti kubwa sana kati ya violwa hivi.
(c) kama ni kiolwa tawala cha obiti yake na hivyo limeondoa violwa vingine kwenye obiti kwa graviti yake.
Ufafanuzi huo uliamuliwa kwakura hata kama wanaastronomia wengine hawakukubali. Azimio hili liliondoa hadhi ya sayari kwaPluto[4] iliyowahi kutazamwa kuwa sayari katika miaka iliyopita.
Wakati mwingine kuna violwa vingine ambavyo vinavyoitwa pia "sayari" ingawa havitoshelezi masharti yote matatu.
Violwa vya angani katikamfumo wa jua letu yenye umbo la kufanana na tufe yasiyolingana na sharti c) huitwa "sayari kibete" - kwa mfano Pluto.
Violwa vinavyozunguka nyota nyingine nje ya mfumo wa jua letu, kama yana masi ya kutosha, huitwa "sayari za nje" (ing.exoplanet). Hadi Mei2016 kuna 2125 zilizotambuliwa[5].
Kwa Kiswahili kuna tofauti kuhusu majina ya sayari kati ya vikundi viwili:
sayari zinazoonekana kwa macho matupu ambazo niUtaridi,Zuhura,Mirihi,Mshtarii naZohali. Hizi zilijulikana tangu kale na mabaharia hasa walizitumia kwa kukadiria njia wakiwa baharini mbali na bara. Majina haya yamepokelewa na Waswahili wa Kale kutoka kwa lugha ya Kiarabu pamoja na majina mengi ya nyota.[6] Ila sayari ya pili yaani Zuhura ambayo ni sayari inayong'aa kuliko zote pia ina jina la Kibantu ambayo ni Ng'andu ("mwenye kung'aa). Kwa lugha za Ulaya kama Kiingereza, Kifaransa, Kijerumani majina ya sayari za jua letu yanatokana na majina yamiungu yaRoma ya Kale auUgiriki ya Kale.
sayari zisizoonekana kwa macho kamaUranus naNeptun pamoja nasayari kibete (Pluto) zilitambuliwa tu bada ya kupatikana kwa mitambo yadarubini. Hatua hii ya kiteknolojia ilitokea Ulaya na hivyo wataalamu wa Ulaya waliendelea katika desturi ya kutumia majina yenye asili katika lugha za kaleKigiriki naKilatini. Elimu ya sayari hizi za nje zilizokuwa geni kwa mataifa yote mengine ya dunia ilisambaa pamoja na majina ya Kiulaya na hivyo lugha nyingi zinatumia majina haya.
Sayari za jua letu
Sayari katika mfumo wa jua,pamoja na nafasi yaCeres
Toka mwaka1930 hadi Agosti2006Pluto ilikuwa ikitambulika kama sayari hivyo kufanya idadi ya sayari zinazojulikana kuwatisa. Hata hivyo chama chenyemamlaka juu ya masuala ya sayari na nyota,Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kimetangaza rasmi kuwa Pluto si sayari na kuiitasayari kibete[7]. Vitabu vingi vya shule vimebadilishwa kulingana na uamuzi huo, japo bado kuna vitabu ambavyo bado vinaonyesha Pluto kuwa sayari kweli.
Sayaritano zaUtaridi,Zuhura,Mirihi,Mshtarii naZohari[8] huonekana kwa macho kamanyota angani. Lakini tangu zamani zilitambuliwa kuwa tofauti kwa sababu hazikai mahali palepale kama nyota ya kawaida bali huhamahama angani. Kutokana na tabia hii zimetazamwa mara nyingi kuwa na nguvu za pekee au hata kuwa miungu.Unajimu umetumia mwendo wa sayari zinazoonekana kwa macho kama msingi muhimu wa makadirio yao.
Sayari nyingine katikamfumo wa jua zimetambuliwa tangu kutokea kwaastronomia yakisayansi kwadarubini. Hizi niUranus naNeptun. Katika lugha ya Kiswahili sayari zinazoonekana kwa macho huwa na majina ya asili yaKiarabu isipokuwa Zuhura ina jina laKibantu laNg'andu pamoja na jina la asili ya Kiarabu. Majina mengine ni ya asili yaKilatini.
Sayari za jua letu hutofautiana kwa ukubwa na muundo.Mshtarii (Jupiter) ni sayari kubwa namasi yake ni mara 318 masi ya dunia yetu. Sayari ndogo niUtaridi na masi yake ni takribannusu ya dunia.
Kutokana na umbali tunatofautisha "sayari za ndani" kuanziaUtaridi (Mercury) hadiukanda wa asteroidi, halafu "sayari za nje" kuanzia Mshtarii (Jupiter) hadi Uranus.
Muundo wa sayari ni tofauti; kuna vikundi kulingana namata inayojenga sayari:
Sayari za mwamba: sayari hizi zina muundo unaofanana na dunia yetu;asilimia kubwa ya masi nimwamba. Hizi ni sayari za ndani za mfumo wa jua letu. Zote ni ndogo kuliko sayari za nje.
Sayari jitu za gesi: sayari hizi kama Mshtarii (Jupiter) na Zohali (Saturn) ni kubwa na zimefanywa nahidrojeni naheli. Masi ya Mshtarii ni mara 318 ile ya dunia, Zohali mara 95. Ilhali sayari hizi nibaridi kutokana na umbali mkubwa na jua, hidrojeni inapatikana kwa kiasi kikubwa katika halimango na kwenye sehemu za ndani hidrojeni ina tabia kamametali kutokana na shinikizo kubwa.
Sayari jitu za barafu: hizi ni Uranus na Neptun. Ni kubwa kuliko dunia, lakini si kama sayari jitu za gesi; Uranus huwa na masi 14 za dunia, Neptun na masi 17 za dunia.Ganda la nje ni mchanganyiko wa hidrojeni namethani, na sehemu za ndani nibarafu ya maji na methani.
Sayari nje ya mfumo wa jua letu
Wataalamu wa astronomia wamegunduasayari-nje (ing.exoplanets) yaani sayari zilizoko nje ya mfumo wa Jua letu zinazozunguka nyota mbalimbali. Kutokana na umbali mkubwa na matatizo ya utazamaji kwa muda mrefu hakukuwa na uhakika kama nyota kuwa na sayari ni jambo la kawaida angani au kama sayari ni chache tu.
Tangu 1995 kuwepo kwa sayari-nje kuliweza kukadiriwa kutokana na mabadiliko ya mwendo wa nyota kadhaa yaliyoweza kuelezwa tu kutokana na masi ya karibu inayobadilisha mwendo wa kawaida. Baada ya kuboreshwa kwa vifaa vipimo vya mabadiliko ya mng'aro vimeonyesha mipito ya sayari, maana wakati wa kupita kwa sayari kati ya nyota fulani na mtazamaji duniani sayari inafunika sehemu ya nyota yake, hivyo mng'aro wake unapungua. Kiasi cha mabadiliko ya mng'aro kinaruhusu kukadiria umbali wa sayari na nyota yake na ukubwa wake. Sayari-nje nyingi zimetambuliwa kwa kutumia mbinu huu. Kutokana na maendeleo ya darubini imewezekana tangu mwaka 2004 kutambua sayari-nje kadhaa moja kwa moja lakini idadi yao hadi sasa ni ndogo wa sababu ugunduzi ni vigumu.
Hadi Aprili 2019 kuwepo kwa sayari-nje 4,048 kumethibitishwa na kati ya hizi mifumo ya sayari 659 imetambuliwa ambako kuna zaidi ya sayari moja.[9]
Nyingi kati ya hizo zilikuwa na ukubwa kufanana na Mshtarii au kubwa zaidi. Lakini sayari ndogo zaidi zimetambuliwa pia.[10]
↑Hizi ni Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii na Zohali. Pale mwanzoni, kabla ya uchunguzi waKopernikus, haikueleweka ya kwamba Dunia ni sayari sawa na hizo nyingine.
↑Azimio 5A ya IAU ya 2006Ilihifadhiwa 20 Januari 2012 kwenyeWayback Machine. "The IAU members gathered at the 2006 General Assembly agreed that a "planet" is defined as a celestial body that (a) is in orbit around the Sun, (b) has sufficient mass for its self-gravity to overcome rigid body forces so that it assumes a hydrostatic equilibrium (nearly round) shape, and (c) has cleared the neighbourhood around its orbit." Tangazo kwenye Tovuti ya IAU, IAU 2006 General Assembly: Result of the IAU Resolution votes, iliangaliwa Mei 2016
↑kuhusu majina ya sayari zilizojulikana kwa Waswahili na hivyo kuwa na majina ya asilia linganisha Jan Knappert, Swahili Islamic poetry, Brill 1971, Vol 1 uk 96-97 - taz google booksearch. Menginevyo kuhusu mchangayiko wa majina ya sayari angalia ukurasa wa majadiliano.
Makala hii kuhusu mambo yasayansi bado nimbegu. Je, unajua kitu kuhusuSayari kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwakuihariri na kuongeza habari.