Movatterモバイル変換


[0]ホーム

URL:


Nenda kwa yaliyomo
WikipediaKamusi elezo ya maandishi huru
Tafuta

Chenene

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Chenene
Chenene wa Kawaida (Gryllotalpa africana)
Chenene wa Kawaida (Gryllotalpa africana)
Uainishaji wa kisayansi
Himaya:Animalia(Wanyama)
Faila:Arthropoda(Wanyama wenye miguu yenye viungo)
Nusufaila:Hexapoda(Arithropodi wenye miguu sita)
Ngeli:Insecta(Wadudu)
Nusungeli:Pterygota(Wadudu wenye mabawa)
Oda:Orthoptera(Wadudu wenye mabawa nyofu)
Nusuoda:Ensifera(Wadudu kamanyenje)
Familia ya juu:Gryllotalpoidea(Wadudu kamachenene)
Familia:Gryllotalpidae(Chenene)
Saussure, 1870
Ngazi za chini

Nusufamilia 2, jenasi 8; jenasi 1 na spishi 17 katika Afrika:

Chenene niwadudu wa jamii yanyenje-ardhi katikafamiliaGryllotalpidae waodaOrthoptera.Miguu ya mbele imetoholewa kwa kuchimba na ina umbo labeleshi lenyemeno.

Maelezo

[hariri |hariri chanzo]

Chenene hutofautiana kwa ukubwa na mwonekano, lakini wengi wana ukubwa wa wastani baini ya wadudu. Kwa kawaida urefu wao ni kati yasm 3.2 na 3.5 katika wapevu. Wametoholewa kwa maisha ya chini yaardhi. Wana umbo lamcheduara na wamefunikwa kwanywele nyingi laini.Kichwa, miguu ya mbele naprotoraksi zinaderaya zito yakhitini, lakinifumbatio ni nyororo kiasi. Kichwa hubebavipapasio viwili kamanyuzi namacho kamashanga ndogo. Jozi mbili zamabawa hufungika bapa juu ya fumbatio. Katika takriban spishi zote mabawa ya mbele ni mafupi na yameviringa, na mabawa ya nyuma ni kamaviwambo na hufikia au kuzidi ncha ya fumbatio. Walakini, katika spishi nyingine mabawa ya nyuma yamepunguka kwa urefu na mdudu hawezi kuruka angani. Miguu ya mbele imekuwa bapa ili kuchimba, lakini miguu ya nyuma imeumbwa kama miguu ya nyenje-ardhi. Walakini, miguu hii imetoholewa zaidi kwa kusukumamchanga badala ya kuruka, ambayo wanafanya mara chache na vibaya.

Mzunguko wa maisha

[hariri |hariri chanzo]

Chenene hupitiametamofosisi isiyo kamili. Mayai hutoatunutu wanaofanana na wapevu isipokuwa kukosa kwa mabawa na viungo vya uzazi. Hupitia mfululizo wa hatua namaambuaji ambazo idadi yao inaweza kufika 10. Pedi za mabawa zinakuza kubwa zaidi baada ya kila ambuaji.

Baada ya kupandana jike anaweza kupitia kipindi chawiki 1-2 kabla ya kutaga mayai. Anachimba ndani ya ardhi kwa kina cha sm 30 (kwenyemaabara sm 72 imeonwa) na kutagakishada cha mayai 25 hadi 60. Kisha jike waNeoscapteriscus hujitoa akiziba kifungu cha kuingilia, lakini katika spishi zaGryllotalpa naNeocurtilla jike ameonekana kubaki katika chumba kinachoungana ili kuchunga kishada. Vishada vingine vinaweza kufuata ndani ya miezi kadhaa kulingana na spishi. Lazima mayai yatagwe kwenye mchanga wenyeunyevu ili kukomaa. Mayai hutoa tunutu katika wiki chache na wakikua hao hula maada yamimea ama chini ya ardhi au juu ya uso wake.

Wapevu wa spishi kadhaa za chenene wanaweza kuhama umbali wa hadikm 8 wakati wa msimu wa uzalishaji. Chenene hukiakia takribanmwaka mzima, lakini katikatabianchi baridi hupitiamajira ya baridi kama tunutu au wapevu wakitulia chini ya ardhi na kuwa wamilifu tena wakati wamajira ya kuchipua.

Mwenendo

[hariri |hariri chanzo]

Wapevu wa spishi nyingi za chenene wanaweza kuruka angani kwa nguvu, ikiwa sio kwa wepesi, lakini madume hufanya hiyo mara chache tu. Kwa kawaida majike huruka juu muda mfupi baada yamachweo na huvutiwa na maeneo ambapo madume hupiga sauti, ambayo hufanya kwa karibu saa moja baada ya machweo. Hii inaweza kuwa ili kupandana au majike wanaweza kuvutiwa na uwepo wa makazi wa kutaga mayai, kama inavyoonyeshwa na idadi ya madume waliopo na kupiga sauti karibu.

Uchimbaji

[hariri |hariri chanzo]
Mguu wa mbele wa chenene: A. Upande wa ndani. B. Upande wa nje. e. Sikio.

Chenene huishi chini ya ardhi takriban saa zote, ambapo huchimba penyo za aina mbalimbalii kwa shughuli kuu za maisha, pamoja na kujilisha, kuwakimbiambuai, kuvutia wenzi (kwa njia ya kupiga sauti), kupandana na kutaga mayai.

Penyo zao kuu hutumiwa kwa kujilisha na kutoroka. Wanaweza kujichimba chini ya ardhi kwa haraka sana na wanaweza kusonga mbele na nyuma katika penyo zilizopo kwa kasi kubwa. Mbinu yao ya kuchimba ni kunanua ardhi pande mbili kwa miguu yao ya mbele yenye nguvu inayofanana na mabeleshi. Miguu hiyo ni mipana na bapa na ina meno na deraya nzito (kutikula ni ngumu na nyeusi).

Mchoro wa dume la chenene akipiga sauti katika upenyo wake.

Madume huvutia wenzi kwa kujenga penyo kwa umbo maalum ambamo hupiga sauti. Upenyo wa spishi zaGryllotalpa una midomo miwili kwenye uso wa ardhi ambayo huongoza katika maumbo yambiu ambayo huunganisha kwenye upenyo mmoja. Kishabalbu inafuata ambayo inavumisha sauti na mbele yake upenyo wa kutoroka. Upenyo aina hii hutumiwa kwa angalau wiki moja. Dume anajiweka kichwa chini na katika balbu, namkia wake uko karibu na panda ya upenyo. Spishi nyingine hujenga mbiu moja inayojifungua nje.

Kupandana hufanyika katika upenyo wa dume. Labda dume atapanua upenyo kumpatia jike nafasi ya kumpanda dume, ingawa katika spishi nyingine mjamiiano hufanyika mkia-mkia. Majike hutaga mayai yao katika penyo zao za kawaida au katika vyumba wanvyochimba kwa kusudi hili. Halafu chumba kinafungwa kabisa kwa kisa cha jenasi yaNeoscapteriscus au kutokufungwa kwa kisa cha jenasiGryllotalpa naNeocurtilla.

Sauti

[hariri |hariri chanzo]

Madume wa chenene hupiga sauti kutoka chini ya ardhi. Kila spishi ina sauti yake ya kipekee. KatikaGryllotalpa gryllotalpa sauti inategemeatoni safi karibu nakHz 3.5 iliyo kubwa ya kutosha ili kufanya ardhi itetemeke sm 20 pande zote za upenyo. KatikaG. africanamarudio ni karibu na kHz 2.34.

Chenene hufanya sauti kama nyenje kwa kukwaruza makali ya nyuma ya bawa la kushoto la mbele, ambalo huundaplectrum, dhidi ya uso wa chini wa bawa la kulia la mbele, ambalo lina safu za meno yasiyo malinganifu; ncha zao zinaelekea nyuma. Plectrum inaweza kusonga mbele kwa nguvu kinzi ndogo, lakini ikisonga nyuma inagusa kila jino, ambayo inasababishamtetemo katika mabawa yote mawili. Sauti inayosababishwa inafanana na matokeo ya kurekebisha sauti safi kwawimbi laHz 66 ili kuunda milio iliyofuatana kwa muda mdogo sawa. Sauti inaweza kulia sana na inaweza kusikika hadi umbali wam 600 kulingana na spishi. Sauti kubwa zaidi zilizopimwa (kwaG. vineae) zilikuwa na nguvu ya wastani yadesibeli 88 kwa umbali wa m 1 kutoka kwa mdomo wa upenyo. Katika mdomo wake sauti inaweza hata kufikia karibu na desibeli 115. Sauti zaG. africana ziko katika mpangilio wa desibeli 94 kwa cm 20 kutoka upenyo.

Koo la mbiu linaonekana kama limerekebishwa ili kufanyia upenyo upeleke sauti vifanisi.Ufanisi huongezeka wakati upenyo ni mnyevu na inasharabu sauti ndogo. Chenene ni wadudu pekee ambao hujengakifaa cha kuzalisha sauti. Kwa kuzingatia usikivu unaojuliwa wa usikiaji wa chenene kwa desibeli 60, jike laG. africana anayeruka usiku angeweza kugundua sauti ya dume kwa umbali wa m 25-30. Hii inalinganishwa na takriban m 5 kwa nyenje wa jenasiGryllus ambaye hajengi upenyo.

Ukubwa wa sauti umeunganishwa na ukubwa wa dume na ubora wamakazi, vitu viwili vilivyoviashirio vya uvutivu wa kiume. Madume wenye sauti kubwa wanaweza kuvutia majike 20 kwa jioni moja, wakati dume wenye sauti ndogo atakosa kuvutia hata mmoja. Tabia hii inawezesha utegaji kwa njia ya sauti. Majike wanaweza kutegwa kwa idadi kubwa kwa njia ya kutangaza sauti ya dume kwa ukubwa wa juu.

Chakula

[hariri |hariri chanzo]

Chenene hutofautiana katikamlo wao. Wengine, kamachenene wa Ulaya, niwalamani na wengine, kamachenene wa kawaida, hula vitu vingi na kujilisha kwamabuu,nyungunyungu,mizizi nanyasi. Spishi chache nimbuai hasa. Huondoka penyo zao usiku ili kutafutamajani namashina ambayo huvuta chini ya ardhi kabla ya kuyala, na pia hula mizizi nainvertebrata chini ya ardhi.

Kama wasumbufu

[hariri |hariri chanzo]

Hasara inayosababishwa na chenene ni hasa matokeo ya shughuli zao za kuchimba. Wakipenya kwenyesentimita chache za juu za udongo, wanasukuma ardhi katikamatuta madogo, ambayo inaongezauvukizaji waunyevu wa uso wa ardhi, kusumbuambegu zinazoota na kuharibu mizizi dhaifu yamiche. Pia wanaharibu nyasi za nyanja na zamachungani kwani wanajilisha kwa mizizi yao na kuifanyia mimea ikauke rahisi na kuharibiwa kwa matumizi.

Katika nchi zao za asili chenene wanamaadui wa asili wanaowadhibiti. Hiyo siyo hivyo ikiwa wamewasilishwa kwa bahati mbaya kwenye sehemu nyingine zadunia. HukoFlorida, kutokamiaka ya 1940 hadi 1980, walizingatiwa wadudu wasumbufu na walielezewa kama “shida kubwa”. Tangu wakati ulemsongamano wa wadudu umepunguka sana.Ripoti yaChuo Kikuu cha Florida kuhusu wadudu hao inadokeza kwamba chenene waNeoscapteriscus waAmerika ya Kusini waliingiaMarekani labda hukoBrunswick, Georgia, katikafarumi yameli kutoka kusini kwa Amerika ya Kusini mnamo 1899, lakini wakati huo ilidhaniwa kimakosa kwamba walitoka kwenyeVisiwa vya Karibi. Utatuzi mmoja unaowezekana ulikuwaudhibiti wa kibiolojia wa wasumbufu kwa kutumianyigukidusiaLarra bicolor. Utatuzi wingine uliotumika kwa mafanikio ni matumizi yanematodi kidusiaSteinernema scapterisci. Wakinyunyiziwa kwenye vishoroba vipitavyo uwanja wa nyasi wanaenea katika machungani yote (na labda mbali zaidi) ndani yamiezi michache ijayo na hawadhibiti chenene sasa hivi tu lakini pia wanabaki tayari kuambukiza katika udongo kwa muda wa miaka kadhaa.

Spishi za Afrika

[hariri |hariri chanzo]

Picha

[hariri |hariri chanzo]
  • Chenene wa Ulaya
    Chenene wa Ulaya
  • Oriental mole cricket (Gryllotalpa orientalis)
    Oriental mole cricket (Gryllotalpa orientalis)
  • Northern mole cricket (Neocurtilla hexadactyla)
    Northern mole cricket (Neocurtilla hexadactyla)
  • Southern mole cricket (Scapteriscus borellii)
    Southern mole cricket (Scapteriscus borellii)
Rudishwa kutoka "https://sw.wikipedia.org/w/index.php?title=Chenene&oldid=1231337"
Jamii:

[8]ページ先頭

©2009-2025 Movatter.jp